Monday, December 29, 2008

Ukweli Kuhusu Mchungaji Mhando Kuanzisha Kanisa Lake La Wasabato Wapentekoste

Nimepokea taarifa za Mchungaji Dakta Herry Mhando kuanzisha kanisa lake la 'Wasabato Wapentekoste' kwa masikitiko. Taarifa hizi zilizoanza kama tetesi na kuthibitishwa kwenye ukurasa wa mbele wa gazeti la Majira la leo zimenisikitisha lakini hazijanishtua.

Zimenisikitisha kwa kuwa ujumbe wa 1994 wa Mchungaji Mhando aliyenihubiri pale Mnazi Mmoja mpaka nikabatizwa baharini feri ni moja ya mibaraka mikubwa ambayo Mungu ametupa wanadamu.

Hazijanishtua kwa kuwa hii sio mara kwanza kwa wahubiri mahiri wa Kiadventista ndani na nje ya Tanzania kufuata mkondo huo.

Pengine kisa cha kusikitisha kuliko vyote vya aina hii katika historia ya kanisa la Kisabato ni kuhusu kilichowatokea wahubiri wawili mahiri baada ya Mkutano Mkuu tete wa kanisa uliofanyika Minneapolis, Minnesota huko Marekani mnamo mwaka 1888.

Mkutano huu wa kihistoria uligubikwa na upinzani mkali hasa kati viongozi wazee wa kanisa na vijana hao wawili wachungaji waliokuwa wakichipukia katika medani ya kuhubiri injili. Vijana hawa, kwa jina Alonzo T. Jones na Ellet J. Waggoner, walikuja na ujumbe ambao wazee hao hasa aliyekuwa Rais wa Mkutano Mkuu wa Kanisa la Kisabato duniani, George I. Butler, na aliyekuwa Mhariri wa gazeti la Review and Heralds na mtunzi wa kitabu maarufu cha Daniel and Revelation(Danieli na Ufunuo), Uriah Smith, waliuona kana kwamba ni ujumbe mpya na usiokubalika kama fundisho la Kibiblia kuhusu wokovu, neema na sheria. Huu ulikuwa ujumbe maridhawa wa Righteousness by Faith, yaani Kuhesabiwa Haki kwa Imani.

Mjumbe wa Mungu, Mama Ellen G. White, alihudhuria mkutano huu na alikubaliana na ujumbe huo ulioibuliwa upya. Baada ya mijadala mikali ujumbe ulipokelewa na kuleta uamsho mkubwa miongoni mwa waadventista. Lakini cha kusikitisha ni kuwa baada ya muda wahubiri A. T Jones na E. J. Waggoner waliachana na kanisa. Jones aliishia kujiunga na kanisa lililojitenga kutoka katika kanisa la Kisabato. Waggoner yeye aliishia kutengana na kanisa baada kuvunja ndoa yake. Kabla ya hapo walijiunga na Dakta John H. Kellog ambaye naye alikuwa ameanza kupingana na imani ya kanisa kwa kufundisha pantheism, yaani 'imani ya uungu katika kila kitu'.

Historia hii ya Jones na Waggoner, pamoja na ya wahubiri wengine maarufu kama Dr. Desmond Ford na Mchungaji Meschack Nyagori, ndio hasa imenifanya nisishtuke kusikia kuwa Mchungaji Mhando ameamua kujitoa katika Kanisa la Waadventista Wasabato "baada ya mafundisho yake yenye miujiza, uponyaji na utajirisho kukataliwa na Kanisa hilo" (Majira 29/12/2008 uk. 4).

Ni kweli kabisa mahubiri ya Mchungaji Mhando katika miaka ya hivi karibuni yamekuwa na ujumbe fulani muhimu kwetu hasa kwetu sisi ambao tulikuwa tunadhani ukristo unaendana na umaskini kana kwamba ukristo = umaskini. Pia ni kweli kabisa kuwa kwa kiasi kikubwa mahubiri yake yalituletea mwamko mkubwa wa kuwa watu wa maombi na watu wa uponyaji hasa ukizingatia kuwa hatukuwa mstari wa mbele katika huduma ya uponyaji. Yote haya ni mafundisho ya Kibiblia kama Agizo Kuu la Yesu Kwetu katika Marko 16:17-18 linavyodhihirisha.

Sasa kama mafundisho hayo yalikuwa ni ya Kibliblia/Kiroho tatizo lilikuwa wapi? Tatizo liko wapi? Hakika tatizo ni kwenye msisitizo. Na suluhisho linapatikana kwenye msingi wa mahubiri.

Pale msisitizo wa injili unapojikita zaidi kwa mwanadamu na mafanikio yake badala ya Mungu na mapenzi yake hapo ndipo panapokuwa na tatizo. Injili inapokuwa ya utajirisho wa mwanadamu zaidi ya inavyokuwa ya ufunuo wa Mungu huo ndio unakuwa mwanzo wa kutengana na ujumbe wa wale mitume waliosema, kwa ujasiri, "imetupasa kumtii Mungu kuliko wanadamu" (Matendo 5: 29). Naam injili inapokuwa ni chakula cha kimwili zaidi ya ilivyo chakula cha kiroho huo ndio unakuwa mwanzo wa kutoungana na neno la Yesu Kristo kusisitiza kuwa "Chakula changu ndicho hiki, niyatende mapenzi yake aliyenipeleka, nikaimalize kazi yake" (Yohana 4: 34).

Kwa kweli sijui ni nini hasa kimemfanya Mchungaji Mhando aanzishe kanisa lake. Zaidi ya yote sijui ni nani hasa amempa hilo agizo - Mungu au Mwanadamu? Ila kama yote yaliyoandikwa katika gazeti la Majira la leo ni ya kweli basi hakika kuna hitaji kubwa la kurejea mafundisho yetu ya msingi ya Kibiblia. Na ni vyema tukafanya hivyo huku tukikumbuka kuwa Mwana wa Mungu mwenyewe alituombea hivi kwa Mungu kabla hata hatujazaliwa na kuwa Wakristo:

"Wala si hawa tu ninaowaombea; lakini na wale watakaoniamini kwa sababu ya neno lao. Wote wawe na umoja; kama wewe, Baba, ulivyo ndani yangu, nami ndani yako; hao nao wawe ndani yetu; ili ulimwengu upate kusadiki ya kwamba wewe ndiwe uliyenituma. Nami utukufu ule ulionipa nimewapa wao; ili wawe na umoja kama sisi tulivyo umoja. Mimi ndani yao, nawe ndani yangu, ili wawe wamekamilika katika umoja; ili ulimwengu ujue ya kuwa ndiwe uliyenituma, ukawapenda wao kama ulivyonipenda mimi" (Yohana 17: 20-22).

AMEN

Wednesday, December 24, 2008

Misheni: Kitovu cha Injili Upareni Suji

"Bali mlango ni mwembamba, na njia imesonga iendayo uzimani, nao waionao ni wachache" - Yesu/Matthayo 7:14
"Njooni kwangu, ninyi nyote msumbukao na wenye kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha" - Yesu/Mathayo 11:28

"Enenda zako; wala usitende dhambi tena" - Yesu/Yohana 8: 11

"Enendeni ulimwenguni mwote, mkaihubiri Injili kwa kila kiumbe" - Yesu/Marko 16:15

"Tena habari njema ya ufalme itahubiriwa katika ulimwengu wote, kuwa ushuhuda kwa mataifa yote; hapo ndipo ule mwisho utakapokuja" - Yesu/Mathayo 24: 14

Maneno Haya - These Words!

"Na maneno haya ninayokuamuru leo, yatakuwa katika moyo wako; nawe uwafundishe watoto wako kwa bidii, na kuyanena uketipo katika nyumba yako, na utembeapo njiani, na ulalapo, na uondokapo.” - Kumbukumbu la Torati 6: 4 – 7

"And these words, which I command you this day, shall be in your heart. And you shall teach them diligently to your children, and shall talk of them when you sit in your house, and when you walk by the way, and when you lie down, and when you rise up." - Deuteronomy 6: 4-7

Adventist Retreat - from Butare to Barraton

Now is the Time! That is the theme of this year's East-Central African Division (ECD) Retreat. The yearly event is currently being held at the University of Eastern Africa, Barraton in Kenya. While we await interesting feedback from those who have been blessed to attend let us photographically relive what transpired in last years retreat at the National University of Rwanda in Butare.
Children also need a treat, a spiritual retreat
Aren't Adventists still the people of the book?

Singing in Tongues, the Rwandese Tongue

Kutoka Kanisani Katesh

"Naam; hamkupata kusoma [Zaburi 8:2], Kwa vinywa vya watoto wachanga na wanyonyao umekamilisha sifa?" -Yesu/Mathayo 21:16

" Waachieni watoto wadogo waje kwangu; wala msiwazuie; kwa maana walio mfano wao hao, ufalme wa mbinguni ni wao" - Yesu/Mathayo 19:16

"Kwa kuwa walipo wawili watatu wamekusanyika kwa jina langu, nami nipo papo hapo katikati yao " - Yesu/Mathayo 18:20