Saturday, March 25, 2017

Somo la 1: Hulka ya Petro

Somo limetafsiriwa na Mgune Masatu

(Luka 5 & 22, Mathayo 14 & 16)

Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2011, Bruce N. Cameron, J.D. Marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya New International Version (NIV), copr. 1973, 1978, 1984 International Bible Society, isipokuwa kama itaelezwa vinginevyo. Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya NIV inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji wa Biblia wa Zondervan. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Somo limekaa kimtazamo kwamba mwalimu anatumia ubao au sehemu nyingine yoyote ambayo inaweza kuonekana na wanafunzi. Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na hukulipata kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza pamoja na lugha nyingine kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.

Utangulizi: Unapomfikiria mwanafunzi Petro, jambo gani linakujia akilini? Ninamfikiria kiongozi – au angalao mtu anayetajwa mara nyingi zaidi ya wanafunzi wengine. Jambo linalojitokeza kutoka kwenye habari zinazomhusu Petro ni kwamba yeye ndiye anayesema, “Hebu tufanye hivi,” au “Naweza kufanya hivi,” lakini baadaye anaishia kuwa na upungufu. Huenda unafahamu kwa kina jinsi mtu anavyojisikia kwa kitendo hiki. Wakati fulani katika maisha ya Petro, baada ya visa vingi tunavyovifahamu ambavyo vilitokea, Petro anabainishwa kama “nguzo” katika kanisa la awali. Wagalatia 2:9. Hamasa kubwa kiasi gani hii! Petro aliandika vitabu viwili katika vitabu vya Agano Jipya, na hilo ndilo somo letu katika robo hii. Hebu tuanze somo letu kwa kuzama kwenye Biblia yetu ili tujifunze zaidi juu ya Petro!

I.                   Petro na Nyavu

A.                Soma Luka 5:1-3. Jaribu kufikiria mwonekano wa tukio hili. Wavuvi wanaosha nyavu zao, wakati watu wanaotaka kusikiliza Yesu akifundisha wamemzunguka wakiwa kundi kubwa. Yesu anafanya nini?

1.                  Kitendo hiki kinakuambia nini kuhusu kama Yesu ni mtu anayetumia akili ya kawaida na mwenye kuendana na uhalisia? (Nadhani hili ni wazo zuri sana na linaloendana na uhalisia.)

2.                  Petro yuko wapi wakati Yesu yumo ndani ya chombo chake akifundisha?  (Yumo ndani ya boti anasikiliza. Yeye haoshi nyavu.)

a.                   Hii inakuambia nini kumhusu Petro? Kwamba ni mvivu? Kwamba kwa ubinafsi wake anawaachia watu wengine wafanye kazi? (Soma Luka 10:39-42. Petro anatenda jambo “jema.” Nahisi hii ilihusisha kazi kubwa kidogo kukifanya chombo kitulie mahali pamoja. Kwa kuongezea, Petro anaonekana kuwa ndiye mmiliki wa chombo, hivyo yumkini anaweza kuwaambia watu wengine waoshe nyavu.)

B.                 Soma Luka 5:4-5. Kama wewe ni mvuvi mahiri, je, unaweza kushawishika kumruhusu mhubiri akwambie namna ya kufanya kazi yako? (Kama viongozi wa kanisa ni wazuri sana kwenye masuala ya biashara basi hilo ni suala gumu. Ukiangalia mifuko ya pensheni inayopendekezwa na kanisa langu kwa waajiriwa wake, mingi kati ya mifuko hiyo ina gharama kubwa kuliko mifuko mingine inayofanana na hiyo. Kwa nini? Bila shaka Petro alijiuliza kuwa, “Mhubiri anajua nini kuhusu uvuvi?” Na kwa kuongezea, Petro alikuwa anafikiria kuwa watatakiwa kuosha nyavu upya.)

C.                 Soma Luka 5:6-7. Hakuna mtu anayeumwa. Hakuna mtu anayekufa. Hakuna anayekabiliana na mdororo wa kifedha. Kwa nini Yesu anatenda huu muujiza? Je, ni malipo kwa kutumia chombo cha Petro?

D.                Soma Luka 5:8-9.  Muujiza huu una athari gani kwenye uhusiano kati ya Yesu na Petro? (Petro anatambua kuwa Yesu ni mtu wa pekee sana.)


1.                  Tafakari jambo hili. Mtazamo gani wa Yesu utamfanya mtu kusema, Ondoka kwangu kwa kuwa mimi ni mtu mwenye dhambi? (Hii inaonekana kama tamko kwamba Yesu ni Masihi. Ikiwa sivyo, basi angalao inamaanisha kuwa Yesu ni mtu mtakatifu sana.)

E.                 Soma Luka 5:10. Unahitimisha nini kutokana na jibu la Yesu, “Usiogope?” (Haya ni maneno tunayoyasoma wakati malaika au Mungu anapomtokea mwanadamu. Angalia, kwa mfano, Mwanzo 15:1. Lazima Petro atakuwa alihitimisha kwamba Yesu ni Masihi.)

F.                  Soma Luka 5:11. Sasa tunaweza kuona kuwa Yesu alikuwa na lengo gani kwa kutenda huu muujiza? (Kumchagua Petro (na Yakobo na Yohana) kama wanafunzi wake.)

1.                  Je, Yesu amekutendea muujiza maishani mwako ili kukuongoza umtumikie?

2.                  Hii inazungumzia nini kuhusu uhusiano wako na Yesu, kwamba alitenda muujiza ili kumshawishi Petro amfanyie kazi?

II.                Petro na Swali

A.                Soma Mathayo 16:13. Unadhani kwa nini Yesu aliwauliza wanafunzi wake swali hili?

B.                 Soma Mathayo 16:14. Ungejisikiaje kutokana na majibu haya endapo ungekuwa Yesu?

C.                 Soma Mathayo 16:15-16. Petro amekuwa na dhana hii tangu lini? (Huenda amekuwa nayo tangu kipindi kile cha muujiza wa uvuvi.)

D.                Soma Mathayo 16:17-19. Kuna mabishano mengi sana juu ya kile ambacho hasa Yesu anakimaanisha. Kama ungekuwa Petro, je, ungelichukulia hili kama jibu chanya? (Naam. Hata kama Yesu anasema kuwa atalijenga kanisa lake kwa imani kwamba yeye ni Kristo, Mwana wa Mungu aliye hai (Jambo ambalo nadhani ndivyo ilivyo), au hata kama anambariki Petro kwa kumpatia mamlaka maalumu, lazima jambo hili linaonekana kuwa jema masikioni mwa Petro.)

E.                 Soma Mathayo 16:20. Kwa nini Yesu anasema hivi? Kama anajali sana hadi kuuliza “Watu hunena Mwana wa Adamu kuwa ni nani?” (Mathayo 16:13), kwa nini basi hataki wanafunzi wake wautangaze ujumbe huo?

F.                  Soma Mathayo 16:21. Unadhani jambo hili linahusiana na kuficha utambulisho wa Yesu? (Bila ya shaka yoyote muda wa matukio haya ni wa muhimu. Endapo wanafunzi wangeanza kuwaambia watu kwamba Yesu ni Masihi, ingeweza kusababisha matatizo kabla ya wakati wake.)

G.                Soma Mathayo 16:22. Unadhani kwa nini Petro alimchukua Yesu pembeni ili kushiriki naye huu ujumbe? (Hakutaka kumwaibisha Yesu mbele ya wanafunzi.)

H.                Soma Mathayo 16:23. Jiweke kwenye nafasi ya Petro. Muda mfupi tu uliopita umembainisha Yesu (kwa usahihi) kuwa ni Kristo, Mwana wa Mungu aliye hai. Mwana wa Mungu anawezaje kuuawa?


1.                  Kibaya zaidi, unawezaje kuitwa “Shetani” kwa kusema kuwa Mwana wa Mungu hatauawa? Unaendelea kumwambia Yesu mambo chanya na ya kumtia moyo! Kwa nini maneno hayo yastahili karipio la kutisha?

I.                   Soma Mathayo 16:24-25, kisha usome sehemu ya mwisho ya Mathayo 16:23. Kuna kosa gani katika mtazamo wa Petro? Tatizo la “Shetani” ni lipi? (Jibu la Yesu linatupatia utambuzi wa fikra ya Petro. Petro alidhani kuwa Mwana wa Mungu alikuwa amekuja kuchukua mamlaka ya taifa lake. Petro alipewa funguo zilizomruhusu kuufunga ulimwengu na mbingu. Jambo hilo linawezaje kuishia kwenye mateso na kifo? “Kamwe halitatokea.” Mathayo 16:22.)

1.                  Kwa nini Yesu hakusema, “Umekosea, Petro,” kwa nini alimuita Petro “Shetani?” Hakuvuka mipaka kwa kusema hivyo? Kwa dhahiri, Petro si Shetani! (Soma tena Mathayo 16:17. Nani aliyemtia moyo Petro hapa? Ni “Baba yangu aliye mbinguni.” Yesu anazungumza kwa usahihi anaposema, “Shetani,” kwa sababu Shetani ndiye aliyemhamasisha Petro kusema “hayo hayatakupata.”)

a.                   Inawezekanaje kwamba kwa dakika moja maneno ya Mungu yanatoka kinywani mwa Petro na dakika inayofuata maneno ya Shetani yanamtoka?

J.                   Kisa hiki kinatufundisha nini kumhusu Petro?

1.                  Hii inatufundisha nini kuhusu sisi? (Tunaweza kupatia kwa usahihi kabisa mambo muhimu ya kiteolojia. Wakati huo huo tunaweza kukosea kabisa jinsi jambo hilo linavyoweza kutenda kazi kwa sababu ya nia zetu za ubinafsi. Tunatakiwa kuwa makini ili kujikinga dhidi ya jambo hili.)

III.             Petro na Maji

A.                Soma Mathayo 14:23-28. Kama kweli Petro ana mashaka kwamba “kivuli” hiki ni Yesu, kwa nini anapendekeza jaribio hili? Kivuli kingeweza kusema, “Naam, njoo.”

1.                  Soma Luka 4:3. Changamoto ya Petro kwa Yesu inatofautianaje na changamoto ya Shetani kwa Yesu kutenda muujiza? Je, Petro kwa mara nyingine tena anazungumza kwa niaba ya Shetani? (Petro ana swali la dhati kabisa. Ombi la muujiza lililoombwa na Petro halikumnufaisha Yesu.)

B.                 Soma Mathayo 14:29-31. Petro aliwezaje, alipokuwa chomboni, kusahau ukweli kwamba upepo ulikuwa unavuma? (Unapojisikia kuwa salama, upepo unaonekana kutokuwa na hatari kubwa.)

1.                  Unadhani Petro angeweza kuogelea? Yeye ni mvuvi! Mafungu haya yanaibua jambo gani zuri kumhusu Petro? (Alimgeukia Yesu ili kupata msaada, hakujaribu kuogelea. Imani yake ilitetereka, lakini utegemezi wake kwa Yesu haukutetereka.)

IV.             Petro na Ukanaji

A.                Yesu amekamatwa (ametiwa mbaroni), na ameanza safari yake kuelekea kwenye mateso. Petro anao ujasiri wa kumfuata Yesu. Soma Luka 22:54-57. Unaelezeaje kitendo cha Petro kusema kuwa hamjui Yesu?

B.                 Soma tena Mathayo 16:21-22. Mambo gani yanatokea katika maisha ya Petro? (Mambo yanakwenda mrama. Inaaminika na watu wengi kwamba Petro ndiye aliyetoa upanga wake kumtetea Yesu wakati wa kukamatwa kwake. Luka 22:49-50. Petro hakupungukiwa ujasiri mambo yalipokuwa yanakwenda vizuri, alipungukiwa ujasiri mambo yalipokuwa hayaendi kwa mujibu wa matarajio yake.)


1.                  Je, hiyo ni kweli kwako pia?

C.                 Rafiki, mojawapo ya mambo makuu kuhusu Yesu kuwa Kuhani wetu Mkuu (Waebrania 7-9) ni kwamba alipitia uzoefu wa maisha ya hapa duniani. Jambo kubwa kuhusu kujifunza vitabu vya Biblia vya Petro ni kwamba tujione wenyewe katika nafasi ya Petro. Je, utadhamiria kujifunza kwa uaminifu maneno ya Petro yaliyovuviwa katika robo hii?


V.                Juma lijalo: Urithi Usioharibika.

No comments:

Post a Comment