Loading...

Saturday, February 14, 2009

Utume wa Mama Ellen G. White

Leo tulikuwa na mjadala mzuri wa Lesoni kuhusu utume wa Mama Ellen G. White katika darasa nalohudhuria katika Kanisa la Waadventista Wasabato Magomeni. Hili ni suala ambalo kwa kawaida huzua mjadala mkali kutokana na kuwepo maoni tofauti kuhusu nafasi na mamlaka ya maandishi yake ukilinganisha na ya Biblia. Nilichojifunza ni kuwa kwa mujibu wa maneno yake mwenyewe, Mama White alikiri kuwa wito wake ulihusisha majukumu mengi zaidi ya jukumu la kuwa nabii. Hakufurahishwa na kuhojiwa kama yeye ni nabii au la na, kwa unyenyekevu, alisema kuwa yeye hajajikweza kujiita kwa cheo hicho. Alichopenda kusisitiza ni kuwa Bwana Mungu alimuita katika ujana wake na kumpa kazi ya kuwa mtume wake ili aufikishe ujumbe wa Mungu kwa watu wake.

Lesoni ya leo imeonesha kuwa utume na ujumbe wa Mama White ulijikita katika dhima kuu ya Injili kama ilivyotabiriwa katika Agano la Kale na kuhubiriwa katika Agano Jipya. Dhima hii ni Mpango wa Mungu wa kumkomboa mwanadamu kutoka kwenye makucha ya dhambi. Msingi wa dhima hii ni Utume/Upatanisho wa Yesu Kristo, Mwana wa Mungu, aliyekuja duniani kuishi kwa ajili yetu, kufa kwa ajili yetu na kufufuka kwa ajili yetu ili kuchukua dhambi za Ulimwengu na kutupatanisha na Mungu. Hivyo, ujumbe wa Mama White haukuwa tofauti na ujumbe wa manabii wengine wa Biblia ambao nao msingi wa ujumbe wao kutoka kwa Mungu ulikuwa Mpango wa Wokovu kupitia Kristo Yesu. Huu ndio msingi wa haya Mafundisho/Imani ya Kisabato.

Licha ya kushabihiana kwa dhima ya utume wa Mama White na dhima ya utume wa manabii wengine wa Mungu, Lesoni pia imeonesha kuwa Mama White pia alipewa jukumu la kuwaonya watu waache dhambi zao za siri. Kama vile Nabii Nathani alivyoagizwa kwenda kumuonya Mfalme Daudi kuhusu dhambi yake aliyokuwa akijaribu kuificha, ndivyo Mama White alivyooneshwa kuhusu dhambi binafsi za watu fulani na kuwaonya kwa faragha watubu. Pia Mama White alitabiri matukio yaliyokuja kutokea kama manabii wengine walivyotabiri. Tukio mojawapo alilooneshwa katika njozi ni kutokea 'Vita ya Wenyewe kwa Wenyewe Marekani', yaani, 'American Civil War' ambapo alitabiri kuwa waumini wenzake watapoteza wana katika vita hiyo. Pia alionya kuwa siku Uprotestanti utakaponyoosha mkono na kukumbatiana na Ukatoliki basi tujue mwisho umekaribia, hali ambayo ilitokea mwaka 1994 lilipotolewa tamko la Evangelicals and Catholics Together: The Christian Mission in the Third Millenium ('Wainjilisti/Waprotestanti na Wakatoliki Pamoja: Utume wa Kikristo Katika Milenia ya Tatu').

Lakini pamoja na vipimo vyote hivi vinavyoonesha kuwa utume wa Mama White ulihusisha kazi ya unabii, uchungaji na uinjilisti, bado waumini wengi hatukubaliani kuhusu mamlaka ya maandishi na unabii wake. Lesoni ya wiki ijayo itakuwa ikijadili suala la mamlaka ya manabii ila kwa leo ninapenda kuhitimisha kwa kusema kuwa kama Roho ya Unabii iliyoongoza manabii wa Biblia na kuwapa ujumbe kutoka kwa Mungu ndio Roho hiyo hiyo ya Mungu iliyomuongoza Mama White na kumpa ujumbe ili awafikishie watu wa Mungu basi hakuna sababu ya kutofautisha mamlaka ya maandishi yake na mamlaka ya maandishi ya manabii wengine. Tukikubaliana kwa hilo basi hatutapata shida ya kutofautisha ujumbe wa 'Nabii'/Mtume' White na ujumbe wa manabii/watume wa Biblia kama tunavyopata sasa hata katika hili Tamko la Kanisa Kuhusu Uhusiano Kati ya Maandishi ya Mama White na Maandishi ya Biblia. Isitoshe Mama White alisema kama maandishi yake yakipingana na Biblia basi Biblia ndio iwe na neno/mamlaka ya mwisho akimaanisha kuwa maandishi yake hayapingani na Biblia. Naam yatapinganaje kama muasisi wake ni mmoja, yaani Yesu aliye "Neno la Mungu" (Yohana 1:1)?

2 comments:

  1. Thank You Sir.
    This is very informative and educational.
    Keep it up.

    ReplyDelete
  2. ni nzuri,inatufundisha mambo mengi muhimu.

    ReplyDelete