Wednesday, April 6, 2011

ALAMA YA NYOKA KATIKA BIBLIA&HISTORIA

Sikuuliza wala kuangalia kama Babu wa Loliondo anakataa sarafu. Mada ya noti ya Shilingi 500 niliileta kama tafakuri tu ndio maana niliweka alama ya kiulizo. Bado natafuta jibu.

Haukuwa mpango wangu kuifanya mada iwe ya kidini. Ila inanibidi nitoe angalizo la Kibiblia. Ili kupata muktadha kamili ni vyema kuchambua alama za Kibiblia kwa kuzingatia vitabu vyote vya Biblia vinavyotaja alama husika na si fungu moja tu au mafungu machache. Kwa maana nyingine, alama ya nyoka inapaswa kuchambuliwa jinsi inavyotumika kuanzia Kitabu cha Mwanzo hadi Ufunuo na asili yake katika muktadha wa Historia na Dini za Misri ya Kale ambako ndiko asili ya 'U-freemason' (kumbuka kisa cha Yusufu, mume wa Binti wa Potifera, Kuhani wa Oni, huko Misri ya Kale, na kikombe cha uaguzi - Mwanzo 44:5; Fimbo ya Haruni iliyogeuka nyoka aliyewameza nyoka wa wachawi na waganga wa Misri ya Kale - Kutoka 7: 8-12; na huu mfano tuliotolewa wa Nyoka wa Shaba Jangwani - Hesabu 21:6-9). Na kabla ya kutumia fungu la Yohana 3:14 linalozungumzia kuinuliwa kwa Yesu kama Musa alivyomuinua nyoka jangwani na kulitumia kujenga hoja kuwa nyoka ni alama ya utabibu Kibiblia, ni muhimu kuchambua maana halisi ya kiroho ya alama hiyo kwa kuzingatia matokeo ya mpango mzima wa imani ya Kibiblia yaliyobainishwa na mafungu haya:

"Bwana Mungu akamwambia nyoka, Kwa sababu umeyafanya hayo, umelaaniwa wewe kuliko wanyama wote...nami nitaweka uadui kati yako na huyo mwanamke, na kati ya uzao wako na uzao wake; huo utakuponda kichwa, na wewe utamponda kisigino"(Mwanzo 3:14-15)

"Joka akamkasirikia mwanamke, akaenda zake afanye vita juu ya wazao wake waliosalia, wazishikao amri za Mungu, na kuwa na ushuhuda wa Yesu..."(Ufunuo 12:17)

"Yule joka akatupwa, yule mkubwa, nyoka wa zamani, aitwaye Ibilisi na Shetani, audanganyaye ulimwengu wote..."(Ufunuo 12:9)

"Akamshika yule joka, yule nyoka wa zamani, ambaye ni Ibilisi na Shetani, akamfunga miaka elfu...asipate kuwadanganya mataifa tena...na yule Ibilisi, mwenye kuwadanganya, akatupwa katika ziwa la moto na kiberiti..."(Ufunuo 20:2,10)

"[Atendaye] dhambi ni wa Ibilisi; kwa kuwa Ibilisi hutenda dhambi toka mwanzo. Kwa kusudi hili Mwana wa Mungu alidhihirishwa ili azivunje kazi za Ibilisi"(1 Yohana 3:8)

"Yeye [Kristo Yesu] asiyejua dhambi alimfanya kuwa dhambi kwa ajili yetu, ili sisi tupate kuwa haki ya Mungu katika Yeye"(2 Wakorintho 5:21)

"Kristo alitukomboa katika laana ya torati, kwa kuwa alifanywa laana kwa ajili yetu; maana imeandikwa, Amelaaniwa kila mtu aangikwaye juu ya mti; ili kwamba baraka ya Ibrahimu iwafikilie Mataifa katika Yesu Kristo, tupate kupokea ahadi ya Roho kwa njia ya imani"(Wagalatia 3:13)

"Na kama kama vile Musa alivyomuinua yule nyoka jangwani, vivyo hivyo Mwana wa Adamu hana budi kuinuliwa; ili kila mtu aaminiye awe na uzima wa milele katika yeye. Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele. Maana Mungu hakumtuma Mwana ulimwenguni ili auhukumu ulimwengu, bali ulimwengu uokolewe katika Yeye"(Yohana 3:14-17) Mchoraji: Lars Justinen

3 comments:

  1. Naam, kwa hiyo tungojee zaidi au ndio mwisho. Ni kuhhusu kikombe cha Babu Loliondo.

    ReplyDelete
  2. babu ni muongo tu.

    ReplyDelete