Wednesday, July 4, 2012

MARY WESEJA MIROBHO KUYENGA (1941 – 2012)



MARY WESEJA MIROBHO KUYENGA (Jan 01, 1941 – June 15, 2012)

Michael: “Nilizunguka Majita na hata Tanzania yote, na sikuweza kupata mchumba mwingine yeyote ambaye angenistahili, isipokuwa Mary Weseja Mirobho. Na hata kama ningeoa mwanamke mwingine awaye yote yule, asingeweza kustahimili dhoruba nilizozipitia mimi katika maisha. Tungeachana tu”. Ndivyo alivyosikika mgane Mchungaji mstaafu Joktan Muura Kuyenga, siku ya Jumamosi ya tarehe 16 Juni, 2012 akishuhudia jambo mojawapo alikumbukalo kumhusu marehemu mke wake, siku moja tu baada ya kifo chake.

Kazi za Maisha

Kulindwa: Mary Weseja Mirobho Kuyenga amekuwa mtumishi wa Mungu na mama mchungaji katika Kanisa la Waadventista wa Sabato Tanzania na nje ya nchi pia. Baadhi ya kazi za utume huu mtakatifu ni pamoja na kuwa:
ü  Katibu muhtasi wa Askofu Mkuu wa Jimbo la Mashariki ya Tanzania (sasa Eastern Tanzania Conference)
ü  Katibu muhtasi wa Askofu Mkuu wa Jimbo la Kusini Magharibi mwa Tanzania (sasa Southern Highlands Conference)
ü  Kiongozi wa Shule ya Sabato Watoto na Vijana Watafuta-Njia chipukizi nchini India na Tanzania
ü  Kiongozi wa Chama cha Wake za Wachungaji katika Jimbo la Mashariki na pia Jimbo Kuu la Tanzania
ü  Katibu Muhtasi wa Idara ya Vijana ya Jimbo Kuu la Tanzania (Tanzania Union)
ü  Mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Arusha, Tanzania, katika fani za Uhazili, hati-mkato, na Usimamizi wa Ofisi
ü  Mama halisi kwa vijana watatu na binti mmoja, wajukuu tisa, na vilevile mchungaji mwenza wa mumewe, yeye akiwa hodari kama mama-mchungaji.

Akishuhudia tabia yake kazini, mmoja wa mzazi-mwenza wa kike amemshuhudia kwa maneno haya, “Hata alipokuwa bado kijana, wakati tukiishi huko Majita, kamwe hukuweza kumsikia huyu mama akishutumiwa kwa masengenyo, ugomvi, wala zahama yoyote ile iliyokuwa ikisikika miongoni mwa wanawake wengine”. Na hivyo ndivyo alivyodumisha haiba yake. Aliendesha kazi zake kwa utulivu na busara, mara kwa mara akiimba wimbo: “Furaha na raha tutapata, Yesu anaporudi”. Utumishi huu ulidhihirika katika mikoa mbalimbali Tanzania, kila mahali akitia fora kama tai hodari arukaye katikati ya dhoruba.

Ndoa na Familia

Heri: Mary alichumbiwa kwa muda mrefu naye Mwinjilisti Joktan Muura Kuyenga. Haikudhaniwa na wasichana wenzake kama kweli Mary alikuwa na viwango alivyovitaka huyu Mwinjilisti “Joki”, kama alivyoitwa siku hizo, kutokana na ustaarabu wake wa kula ugali kwa kutumia uma (“masakiko”) na kisu. Japo Waswahili wasema fimbo ya mbali haiui nyoka, Mchungaji Kuyenga alimaliza masomo yake nchini Uganda, kisha hawa njiwa wawili wapendanao wakaunganishwa katika ndoa takatifu ya Ki-kristo tarehe 15 Januari, 1963 huko kwao binti, Iramba-Majita, mkoani Mara. Ndoa ilifungwa na hayati Mch. Daniel Mutani Yangwe. Miaka ya 1965, 1966, 1968 na 1971 walizaliwa kwao wana na binti, ambao wote walifuata nyayo za wazazi wao, na kuwa wachungaji katika Kanisa la Waadventista wa Sabato, naye binti kuolewa na mchungaji. Kuyathibitisha Maandiko Matakatifu ya Sulemani kuwa ya kweli, naam, hata kumhusu Mary Weseja Mirobho Kuyenga, “Wanawe huondoka na kumwita ‘Heri’; Mumewe naye humsifu na kusema, ‘Binti za watu wengi wamefanya mema, Lakini wewe umewapita wote’” (Mithali 31:28-29). Isingalikuwa kunyakuliwa kwa mauti, Mary Na Joktan Kuyenga wangalisherehekea jubilei ya miaka 50 ya ndoa.

Chanzo cha Kifo

Deborah: Mchungaji Joktan Kuyenga, baada ya kushuhudia mateso apatayo mgonjwa wa kifua (asthma), alimsihi Mungu kwamba yeye atakapooa, aepushwe na mwenzi mwenye huo ugonjwa. Lakini Mungu si Athumani wala Yohane; muda mfupi sana baada tu ya kufunga ndoa, mwali wake alibanwa na kifua. Hata hivyo, kwa mkono wa BWANA na utaalamu wa utabibu, Mary alifanyiwa upasuaji kule Heri Mission Hospital, Kigoma, upasuaji ambao ulimpumzisha kabisa maradhi ya kubanwa kifua kwa muda wa miaka 40. Mwaka 2006 Mary aliibukiwa upya kwa mateso ya kifua, ambayo yaliibua pia masumbufu ya mapafu, vali ya moyo, figo, ini, na mirija ya uzazi. Katika hatua za mwishoni kabisa, ushauri wa utabibu uliondoa vilevile uwezekano wa upasuaji. Mary alipata ahueni fupi kwa kutumia madawa mbalimbali, hata hivyo miaka yake 70 ongeza mmoja aliyokuwa amepangiwa na Mwenyezi ilikuwa imetimia. Kwa utulivu wa matumaini tele ndani Yake Bwana na Mwokozi wake, Mary alipumua pumzi yake ya kutuaga, akiwa mikononi mwa binti wake wa pekee aliyekuwa tabibu wake nyumbani.

Hitimisho

Michael: Mary Weseja Mirobho Kuyenga ni jemadari aliyelala usingizi wa mauti. Baada ya mapambano makali lakini ya ushindi wenye kishindo kilichosikika mbinguni na akhera – shujaa, mama katika Israeli, amepumzika.
Ameweka silaha chini – shujaa hodari katika vita ya wema na uovu
Ameweka silaha chini – tai aliyetawala anga kwa ustadi wa mwanamke mchaji wa Mungu
Ameweka silaha chini – siyo kwa woga ama kukata tamaa, bali kwa kuipokea mede ya ushindi
Ameweka silaha chini – mama wa kweli katika Israeli
Ameweka silaha chini – ayala apendezaye, waridi la upendo halisi
Ameweka silaha chini – miguuni Pake Jemadari Mkuu Yesu Kristo aliyemuita ubavuni Mwake.
Ameweka silaha chini – hadi hapo tutapoisikia parapanda ya ufufuo!

Nasi leo twasherehekea kumbukumbu ya huyu hodari wa msalaba, tukilishangilia tumaini lile lenye baraka: “tazama Yuaja na mawingu, na kila jicho litamwona”, ndiyo, pamoja na lile la Mary Kuyenga.
Tuonane pale, Yesu Anaporudi.
-         
Imeandaliwa na Heri Gidion Kuyenga, Debora Nyamujungu Mang’ombe, Harun Kuliundwa Kuyenga, Michael Magesa Kuyenga.

2 comments:

  1. Poleni wapendwa kwa kifo cha mama. Hakika makala yeunu ni ya maombolezo ya mama yenu mpenzi. Mungu awafariji nyote hasa mgane aliyeachwa na mkeo.

    ReplyDelete
  2. Hakika mameno haya yafaa kuwa fundisho na kuwageuza watu wote hususan wana wa kike kumjua Mungu na kuwafanya waume zao wamgeukie Mungu.Poleni sana.

    ReplyDelete