Michael: “Nilizunguka Majita
na hata Tanzania yote, na sikuweza kupata mchumba mwingine yeyote ambaye
angenistahili, isipokuwa Mary Weseja Mirobho. Na hata kama ningeoa mwanamke
mwingine awaye yote yule, asingeweza kustahimili dhoruba nilizozipitia mimi
katika maisha. Tungeachana tu”. Ndivyo alivyosikika mgane Mchungaji mstaafu
Joktan Muura Kuyenga, siku ya Jumamosi ya tarehe 16 Juni, 2012 akishuhudia
jambo mojawapo alikumbukalo kumhusu marehemu mke wake, siku moja tu baada ya
kifo chake.
Kazi
za Maisha
Kulindwa:
Mary Weseja Mirobho Kuyenga amekuwa mtumishi wa Mungu na mama mchungaji katika
Kanisa la Waadventista wa Sabato Tanzania na nje ya nchi pia. Baadhi ya kazi za
utume huu mtakatifu ni pamoja na kuwa:
ü
Katibu muhtasi wa Askofu Mkuu wa Jimbo la
Mashariki ya Tanzania (sasa Eastern Tanzania Conference)
ü Katibu
muhtasi wa Askofu Mkuu wa Jimbo la Kusini Magharibi mwa Tanzania (sasa Southern
Highlands Conference)
ü Kiongozi
wa Shule ya Sabato Watoto na Vijana Watafuta-Njia chipukizi nchini India na
Tanzania
ü Kiongozi
wa Chama cha Wake za Wachungaji katika Jimbo la Mashariki na pia Jimbo Kuu la
Tanzania
ü Katibu
Muhtasi wa Idara ya Vijana ya Jimbo Kuu la Tanzania (Tanzania Union)
ü Mhadhiri
katika Chuo Kikuu cha Arusha, Tanzania, katika fani za Uhazili, hati-mkato, na
Usimamizi wa Ofisi
ü
Mama halisi kwa vijana watatu na binti mmoja,
wajukuu tisa, na vilevile mchungaji mwenza wa mumewe, yeye akiwa hodari kama mama-mchungaji.
Akishuhudia tabia yake kazini, mmoja wa mzazi-mwenza wa kike
amemshuhudia kwa maneno haya, “Hata alipokuwa bado kijana, wakati tukiishi huko
Majita, kamwe hukuweza kumsikia huyu mama akishutumiwa kwa masengenyo, ugomvi,
wala zahama yoyote ile iliyokuwa ikisikika miongoni mwa wanawake wengine”. Na
hivyo ndivyo alivyodumisha haiba yake. Aliendesha kazi zake kwa utulivu na
busara, mara kwa mara akiimba wimbo: “Furaha na raha tutapata, Yesu anaporudi”.
Utumishi huu ulidhihirika katika mikoa mbalimbali Tanzania, kila mahali akitia
fora kama tai hodari arukaye katikati ya dhoruba.
Ndoa
na Familia
Heri:
Mary alichumbiwa kwa muda mrefu naye Mwinjilisti Joktan Muura Kuyenga.
Haikudhaniwa na wasichana wenzake kama kweli Mary alikuwa na viwango
alivyovitaka huyu Mwinjilisti “Joki”, kama alivyoitwa siku hizo, kutokana na
ustaarabu wake wa kula ugali kwa kutumia uma (“masakiko”) na kisu. Japo
Waswahili wasema fimbo ya mbali haiui nyoka, Mchungaji Kuyenga alimaliza masomo
yake nchini Uganda, kisha hawa njiwa wawili wapendanao wakaunganishwa katika
ndoa takatifu ya Ki-kristo tarehe 15 Januari, 1963 huko kwao binti,
Iramba-Majita, mkoani Mara. Ndoa ilifungwa na hayati Mch. Daniel Mutani Yangwe.
Miaka ya 1965, 1966, 1968 na 1971 walizaliwa kwao wana na binti, ambao wote
walifuata nyayo za wazazi wao, na kuwa wachungaji katika Kanisa la Waadventista
wa Sabato, naye binti kuolewa na mchungaji. Kuyathibitisha Maandiko Matakatifu
ya Sulemani kuwa ya kweli, naam, hata kumhusu Mary Weseja Mirobho Kuyenga,
“Wanawe huondoka na kumwita ‘Heri’; Mumewe naye humsifu na kusema, ‘Binti za
watu wengi wamefanya mema, Lakini wewe umewapita wote’” (Mithali 31:28-29). Isingalikuwa
kunyakuliwa kwa mauti, Mary Na Joktan Kuyenga wangalisherehekea jubilei ya
miaka 50 ya ndoa.
Chanzo
cha Kifo
Deborah:
Mchungaji Joktan Kuyenga, baada ya kushuhudia mateso apatayo mgonjwa wa kifua
(asthma), alimsihi Mungu kwamba yeye atakapooa, aepushwe na mwenzi mwenye huo
ugonjwa. Lakini Mungu si Athumani wala Yohane; muda mfupi sana baada tu ya
kufunga ndoa, mwali wake alibanwa na kifua. Hata hivyo, kwa mkono wa BWANA na
utaalamu wa utabibu, Mary alifanyiwa upasuaji kule Heri Mission Hospital,
Kigoma, upasuaji ambao ulimpumzisha kabisa maradhi ya kubanwa kifua kwa muda wa
miaka 40. Mwaka 2006 Mary aliibukiwa upya kwa mateso ya kifua, ambayo yaliibua
pia masumbufu ya mapafu, vali ya moyo, figo, ini, na mirija ya uzazi. Katika
hatua za mwishoni kabisa, ushauri wa utabibu uliondoa vilevile uwezekano wa
upasuaji. Mary alipata ahueni fupi kwa kutumia madawa mbalimbali, hata hivyo
miaka yake 70 ongeza mmoja aliyokuwa amepangiwa na Mwenyezi ilikuwa imetimia.
Kwa utulivu wa matumaini tele ndani Yake Bwana na Mwokozi wake, Mary alipumua
pumzi yake ya kutuaga, akiwa mikononi mwa binti wake wa pekee aliyekuwa tabibu
wake nyumbani.
Hitimisho
Michael:
Mary Weseja Mirobho Kuyenga ni jemadari aliyelala usingizi wa mauti. Baada ya
mapambano makali lakini ya ushindi wenye kishindo kilichosikika mbinguni na akhera
– shujaa, mama katika Israeli, amepumzika.
Ameweka silaha chini – shujaa hodari katika vita ya wema na uovu
Ameweka silaha chini – tai aliyetawala anga kwa ustadi wa mwanamke
mchaji wa Mungu
Ameweka silaha chini – siyo kwa woga ama kukata tamaa, bali kwa
kuipokea mede ya ushindi
Ameweka silaha chini – mama wa kweli katika Israeli
Ameweka silaha chini – ayala apendezaye, waridi la upendo halisi
Ameweka silaha chini – miguuni Pake Jemadari Mkuu Yesu Kristo
aliyemuita ubavuni Mwake.
Ameweka silaha chini – hadi hapo tutapoisikia parapanda ya ufufuo!
Nasi leo twasherehekea kumbukumbu ya huyu hodari wa msalaba,
tukilishangilia tumaini lile lenye baraka: “tazama Yuaja na mawingu, na kila
jicho litamwona”, ndiyo, pamoja na lile la Mary Kuyenga.
Tuonane pale, Yesu Anaporudi.
-
Imeandaliwa na Heri Gidion Kuyenga, Debora
Nyamujungu Mang’ombe, Harun Kuliundwa Kuyenga, Michael Magesa Kuyenga.